NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA TANO
NOVENA YA HURUMA YA MUNGU SIKU YA TANO, JUMANNE BAADA YA PASAKA
Novena hii pia inaweza kusaliwa wakati wowote na katika kipindi chochote cha mwaka lakini inapendekezwa Novena ianzwe katika siku ya Ijumaa.
Tujiandae kusali kwa kuanza na sala za awali kama vile Uje Roho Mtakatifu pamoja na Sala ya kutubu kisha tuendelee kama inavyoonyeshwa hapa chini:
Maneno ya Mkombozi: “Leo niletee roho za NDUGU WALIOJITENGA NA KANISA, na uwazamishe katika Bahari Kuu ya Huruma yangu. Wakati ule wa mateso yangu makali, watu hawa waliurarua mwili wangu na roho yangu, yaani Kanisa langu. Pindi warudipo tena katika Umoja wa Kanisa, majeraha yangu hupona, na kwa njia hii wanapunguza ukali wa mateso yangu”.
Kiongozi: Tuwaombee wale waliopotoka katika Imani Katoliki na kujitenga na Kanisa.
Wote: Ee Yesu Mpole na mwenye Huruma, Wewe u Huruma na Wema wenyewe, hukatai kuwapa mwanga wale wote wanaoutafuta. Uzipokee ndani ya Moyo wako wenye Huruma, roho za ndugu zetu waliojitenga. Uwavute kwa mwanga wako, ili warudi tena katika Umoja wa Kanisa lako Takatifu, na uwadumishe humo, wasiweze kutoroka tena Moyo wako wenye Huruma sana, bali uwawezeshe wao pia pamoja nasi, kuusifu na kuutukuza ukarimu wa Huruma Yako Kuu, kwa milele na milele. Amina.
Baba yetu ……. Salamu Maria …….. Atukuzwe …………..
Wote: Baba wa Milele, uzielekee kwa macho ya huruma, roho za ndugu zetu waliojitenga na Kanisa lako Takatifu, hasa wale waliozitapanya Baraka zako na kuzitumia vibaya neema zako, kwa kuendelea kishupavu katika mafundisho yao ya upotofu. Usiyaangalie hayo makosa yao, bali uutazame upendo wa Mwanao Mpenzi, pamoja na mateso yake makali aliyovumilia kwa ajili yao. Watu hawa pia, wameingizwa ndani ya Moyo wa Yesu Mwanao, wenye Huruma Kuu. Uwawezeshe vile kwamba, wao pamoja na sisi sote, tuisifu na kuitukuza Huruma Yako Kuu, kwa milele na milele. Amina.
Tumia Rozari ya kawaida kusali Rozari ya Huruma ya Mungu kama ifuatavyo:
Baba yetu … Salamu Maria …. X3 Nasadiki kwa Mungu Baba Mwenyezi …….
Kila penye punje kubwa (Badala ya Baba yetu):
Baba wa Milele, ninakutolea Mwili na Damu, Roho na Umungu, wa Mwanao Mpenzi sana, Bwana wetu Yesu Kristu, kwa ajili ya malipizi ya dhambi zetu, na dhambi za dunia nzima.
Kila penye punje ndogo (badala ya Salamu Maria):
Mwanzishaji: Kwa ajili ya mateso makali ya Bwana wetu Yesu Kristu,
Wote huitika: Utuhurumie sisi na dunia nzima.
Mwisho wa Rozari sali mara tatu sala ifuatayo:
Mungu Mtakatifu,
Mtakatifu mwenye Enzi,
Mtakatifu unayeishi milele,
Utuhurumie sisi na dunia nzima (x3).
LITANIA YA HURUMA YA MUNGU
Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utuhurumie – Kristu utuhurumie
Bwana utuhurumie – Bwana utuhurumie
Kristu utusikie – Kristu utusikilize
Baba wa mbinguni Mungu – utuhurumie
Mwana Mkombozi wa dunia Mungu - utuhurumie
Roho Mtakatifu Mungu - utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu mmoja – utuhurumie.
Huruma ya Mungu iliyo sifa kuu ya Muumba wetu - Tunakutumainia (iwe kiitikio)
Huruma ya Mungu iliyo kilele cha ukamilifu wa Mwokozi wetu
Huruma ya Mungu iliyo upendo usiopimika wa Roho Mtakasa
Huruma ya Mungu fumbo lisilofahamika la Utatu Mtakatifu
Huruma ya Mungu iliyo ishara ya uwezo mkuu wa Mungu Mwenyezi
Huruma ya Mungu iliyofumbuliwa katika kuziumba Roho za Malaika wa mbinguni
Huruma ya Mungu iliyotuumba na kutuamuru tuwepo bila kutokana na chochote
Huruma ya Mungu inayotujalia maisha ya kutokufa
Huruma ya Mungu inayotukinga na adhabu tunazostahili
Huruma ya Mungu inayotuinua tutoke katika taabu, unyonge na maumivu ya dhambi zetu
Huruma ya Mungu inayotufanya wenye haki katika Neno aliyejifanya Mtu
Huruma ya Mungu inayofurika kutoka katika majeraha ya Kristu
Huruma ya Mungu inayobubujika kutoka ndani ya Moyo Mtakatifu wa Yesu
Huruma ya Mungu iliyotupatia Bikira Maria Mtukufu awe kwetu Mama wa Huruma
Huruma ya Mungu iliyoonyeshwa katika kuanzishwa Kanisa Katoliki
Huruma ya Mungu inayopatikana katika mafumbo ya Sakramenti Takatifu
Huruma ya Mungu inayotolewa kwa wanadamu wote kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na Kitubio
Huruma ya Mungu inayotolewa katika Sakramenti ya Ekaristi na Upadrisho
Huruma ya Mungu inayoonyeshwa kwetu pale inapotuita na kutuingiza katika kuwatakatifuza wenye haki
Huruma ya Mungu inayotimilika katika ukamilifu wa watu watakatifu
Huruma ya Mungu chemchemi ya afya kwa wagonjwa na wote wanaoteseka
Huruma ya Mungu iliyo faraja ya wote wenye uchungu moyoni
Huruma ya Mungu iliyo tumaini la roho zinazosumbuliwa na mkato wa tamaa
Huruma ya Mungu iliyo mwenzi wa daima na popote wa watu wote
Huruma ya Mungu inayowahi kutuletea neema zake
Huruma ya Mungu iliyo amani yao wanaokufa
Huruma ya Mungu iliyo burudisho na faraja yao marehemu wa toharani
Huruma ya Mungu iliyo furaha ya mbinguni kwa watakatifu wote
Huruma ya Mungu iliyo taji la watakatifu wote
Huruma ya Mungu chemchemi ya miujiza isiyokauka
Mwanakondoo wa Mungu uliyetuonyesha huruma yako kuu katika kuikomboa dunia kwa msalaba wako mtakatifu, - utusamehe ee Bwana
Mwanakondoo wa Mungu unayejitolea kwetu kwa mapendo na huruma katika kila adhimisho la Sadaka ya Misa Takatifu,- utusikilize ee Bwana
Mwanakondoo wa Mungu anayeondoa dhambi za dunia kwa njia ya huruma yako isiyo na mwisho,- utuhurumie.
Kiongozi : Bwana utuhurumie –
Wote: Kristu utuhurumie, Bwana utuhurumie.
Kiongozi : Huruma anana za Bwana zi juu ya kazi zake zote –
Wote: Huruma za Bwana nitaziimba milele.
Tuombe: Ee Mungu uliye na huruma isiyo na mwisho, na hazina za wema na upendo wako hazina mipaka. Tunakusihi ututazame sisi watu wako huku duniani na kutuongezea huruma yako tena na tena, ili itusaidie tusije tukakata tamaa hata mara moja, haidhuru tukumbane na majaribu makubwa kiasi gani, bali tuweze daima kuzielekea na kuzishika amri zako, kwa matumaini na kutimiza mapenzi yako matakatifu, ambayo ndiyo huruma yenyewe. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristu Mwanao, Mfalme wa Amani na Huruma, aishiye na kutawala nawe, na Roho Mtakatifu, kwa pamoja mkituonyesha huruma, daima na milele. Amina.
Comments
Post a Comment